Na Mwandishi wetu.
Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Bi. Mwamvita Makamba amewataka wanawake wajasiriamali hususan wadogo kutambua kuwa maendeleo ya biashara zao na hatimae hali zao za kiuchumi kutategemea pamoja na mambo mengine namna wanavyotumia vizuri fursa za uwezeshaji wanazotengenezewa.Bi. Mwamvita ametoa changamoto hiyo Wilayani Simanajiro, Mkoani Manyara katika kijiji Cha Mirerani wakati akikabidhi mikopo isiyo na riba wala dhamana yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni Tisa kwa vikundi tisa vya akina mama iliyotolewas na mradi wa Vodacom wa kusaidia wajasiriamali wadogo wanawake wa MWEI.
Bi. Mwamvita amesema kadiri ambavyo wanawake watakuwa tayari kutumia vema fursa wanazotengenezewa ikiwemo ya MWEI wanajiweka katika nafasi nzuri ya kujiwezesha kiuchumi na kuondokana na dhana kwamba mwanamke ni kiumbe tegemezi.
“Wanawake wenzangu leo Vodacom inapowakabidhi mikopo isiyo na riba wala dhamana ni fursa adhimu sana kwenu, ni wajibu wenu kutumia vema fursa hii kujiinua kama ilivyokuwa wajibu wa Vodacom kuwatafuta, kuwafikia na kuwawezesha, kazi sasa ni kwenu”Alisema Bi. Mwamvita.
Bi. Mwamvita amesema kumekuwepo na kilio kikubwa cha wanawake wajasiriamali wadogo kutofikiwa kwa urahisi ama kukosa uwezo wa kukopesheka kutoka taasisi za fedha, hivyo katika kutimiza azma ya kubadili maisha ya watanzania Vodacom ilibuni mradi wa MWEI kutatua changamoto hiyo.
“Ni vigumu kupata taasisi itakayokukopesha mfnyabishara wa vitumbua, genge mchuuzi wa samaki, msusi n.k tena bila riba wala dhamana na zaidi kukupatia mafunzo ya ujasiriamali kwa gharama zake, Vodacom licha ya kwamba biashara yetu ni huduma za simu imethubutu kubuni mradi wa mikopo kwa kuwa inapenda kuona maisha ya watanzania wakiwemo akina mama yanabadilika”Aliongeza Mwamvita
Aidha Bi. Mwamvita amewataka wanawake hao kuhakikisha mikopo waliyoichukua inleta tija katika biashara zao hasa kuinua mitaji ili nao waweze kusimama na kusaidia wanawake wengine.
“Kabla ya kuwakibidhi mikopo hii tumewapatia mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo somo la utunzaji wa mahesabu ya biashara, tutumie elimu hiyo na mikopo hii kujiimarisha ili kuinua sauti zetu kwenye jamii”Aliongeza Mwamvita huku akisindikizwa na vigelegele vya furaha kutoka kwa akina mama.
Mradi wa MWEI ni mahsusi kwa ajili ya kusaidia akina mama nchini kama mchango wa Vodacom kuunga mkono juhudi za kitaifa za kumwezesha kiuchumi mwanamke wa kitanzania na unalenga hasa wanawake wenye biashara zenye mitaji ya kati ya Sh. 5000 na 200,000
Bi. Mwamvita amesema kuwa mradi wa MWEI umejiwekea lengo la kuwafikia wanawake wengi zaidi hususan maeneo ya vijijini ambao pamoja na kujituma katika bishara ndogondogo wanakabiliw ana uchache wa fursa za uwezeshaji.
“Ni hatua muhimu katika maisha yetu kama Vodacom kusaidia ujenzi wa ustawi wa jamii hapa nchini, tuna namna nyingi ya kubadili maisha ya watanzania kama dira yetu invyosema, MWEI ni namna mojawapo”. Alisema Mwamvita.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa mikopo hiyo mbali na kuishukuru Vodacom, wanufaika hao wameahidi kuitumia vizuri mikopo hiyo ili kutimiza malengo ya kibiashara waliyonayo.
“Wengi wetu hapa ni wajasiriamali wadogo tunaojishughulisha na biashara za ususi, mama lishe n.k changamoto kubwa tuliyokuwa tukikabiliana nayo ni kuweza kufikiwa na mikopo nafuu, leo tunafuraha kuona tumepata mikopo isiyo na riba hata shilingi moja” Alisema Johari Mwaselela Mmoja wa viongozi wa Vikundi.
Amesema kupitia vikundi vyao, watahakikisha wanafanya kazi kwa pamoja na kuhimizana ili mikopo waliyopatiwa itoe tija ya kuinua mitaji yao, wakuze faida sambamba na kusaidia kubadili hali zao za maisha.
Tunawaomba Vodacom kama mlivyotufikia sisi hapa kijijini muwafikie na wenzetu wengine waliopo vijijini kama sisi na muwaokoe, kwa kweli wanawke bado tupo nyuma, tunawashukuru sana MWEI.”Aliongeza Mamam Mwaselela.
Awali Meneja wa Mradi wa MWEI Bi Mwamvua Mlangwa alisema hadi kufikia Januari mwaka huu kiasi cha Shilingi 150 Milioni kimeshatolewa na kunufaisha akina mama zaidi ya 6,000
Bi. Mwamvua amesema idadi ya wanaohitaji mikopo hiyo ni kubwa hivyo amewasihi kina mama hao wa Mirerani kutumia vizuri fursa hiyo na kuhakikisha wanarudisha mikopo kwa wakati ili kuwafikia wanawake wa sehemu nyengine nchini.
Kupitia mradi wa MWEI Vodacom huvipatia vikundi vya akina mama mikopo pamoja na mafunzo ya ujasiriamali kazi ambayo hufanywa na Shirika la kuhudumia viwanda Vidogo – SIDO kwa gharama za Vodacom.
Mikoa ya Arusha, Manyara, Morogoro, Tanga, Rukwa na Katavi, Dodoma, Mara, Mwanza,Shinyanga na Pwani imeshanufaika na mikopo ya MWEI tangu mradi huo ulipoanzishwa mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment